Friday, August 21, 2009

Wabunge CCM waivimbia Nec


WASEMA HAWATAKOMA KUPAMBANA NA UFISADI


Leon Bahati na Exuper Kachenje


SIKU chache baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kuwaonya wanachama wanaopambana na mafisadi hadharani, wabunge kadhaa wa chama hicho wamesema hawatasalimu amri na badala yake wataendelea kupinga ufisadi popote bila kujali onyo hilo.


Wakati wabunge hao wakiitunishia misuli Nec, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Milton Makongoro Mahanga amefurahia uamuzi wa Nec akisema umetolewa kwa kadri alivyotarajia.


Wakizungumza na Mwananchi wabunge ambao wamekuwa wakitoa tuhuma mbalimbali za ufisadi ndani na nje ya Bunge walisema wataendelea 'kufa' na mafisadi na kwamba tamko hilo kamwe haliwezi kuwatisha.


Nec ilitoa tamko Agosti 17 mwaka huu baada ya kumaliza kikao chake mjini Dodoma, ikipiga marufuku viongozi na wanachama wake kuishambulia serikali bungeni, ikidai kuwa vita ya ufisadi ni ya chama na si ya kikundi cha watu wachache ndani ya chama hicho. Nec iliunda timu ya watu watatu kuwafuatilia wabunge wenye tabia hiyo.


Mkutano huo pia ulimweka kitimoto spika wa Bunge, Samuel Sitta huku wajumbe wakitaka anyang'anywe kadi yake ya uanachama kwa madai kuwa ana ruhusu na kushabikia mijadala inayoiweka serikali kwenye hali ngumu.


Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro, mmoja wa wabunge wanaotaka suala la tuhuma dhidi ya rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuhusu mgodi wa Kiwira lishughulikiwe, alisema: "Sidhani kama kuna mtu amefungwa mdomo na Nec.


Mdomo upo palepale na watu wataendelea kuongea. Nec haiwezi kumfunga mdomo spika wala wabunge. Haya ni mabadiliko muhimu ambayo CCM lazima ipitie ili kuondoa rushwa.".


Mbunge huyo kutoka mkoa ambao CCM imekuwa ikipata shida kwenye uchaguzi, alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni zake hakuna mtu nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano mwenye uwezo wa kumfunga mdomo spika wala wabunge kuzungumzia ufisadi, isipokuwa bunge lenyewe.


Alisisitiza kuwa, ili CCM iondoe rushwa nchini na ambayo hata Rais Jakaya Kikwete anakiri kuwa ipo, lazima ikubali kupitia kipindi hiki ambacho kitaendelea kuwepo mpaka mambo yatakapokaa sawa hapo baadaye.


"Tumeisikia Nec, lakini wavumilie tu kwani lazima mabadiliko yatokee. Wananchi ndio wenye chama na ndio wanaotaka wabunge wao wapambane na uovu na ufisadi," alisema Kimaro.


Alisema ni lazima watuhumiwa wa rushwa wafikishwe mahakamani.


Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ambaye pia ni mmoja wa vinara wa vita dhidi ya ufisadi, aliwataka wananchi kuondoa shaka kuhusu uamuzi huo wa Nec akisema kuwa wao kama wabunge wako imara na wataendelea kutetea maslahi ya wananchi bila kuogopa.


"Katiba ya CCM inaeleza vizuri kuhusu ufisadi na inaeleza wazi kwamba rushwa ni adui wa haki. Pia inakataza mtu kutumia cheo chake ili kujinufaisha," alisema Ole-Sendeka na kuongeza kuwa tayari kifungu hicho kimempa rungu dhidi ya mafisadi.


Ole-Sendeka alisema alikuwa hajasoma magazeti ili kuona maazimio hayo ya Nec, lakini anaamini kuwa CCM imeweka misingi ya kupambana na rushwa hivyo hakuna kitakachomzuia kusema ukweli kwa manufaa ya wananchi.


Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo ambaye alisema kama wabunge wakikaa kimya katika maslahi ya nchi, watakuwa hawawatendei haki wananchi ambao wanawawakilisha na kuwatetea mbele ya serikali.


Alitoa mfano wa suala ambalo wabunge hawatarudi nyuma katika kuibana serikali kuwa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya utoaji wa zabuni ya umeme wa dharura kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC.


Katika sakata hilo, kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ilitoa ripoti iliyomtaja waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kusababisha ajiuzulu na baadaye kufuatiwa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha.


Bunge pia lilipitisha maazimio ambayo baadhi hayajatekelezwa, kiasi cha kuufanya mkutano uliopita uiagize serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezwaji wa maazimio hayo kwenye mkutano ujao wa Novemba.


Kwa upande mwingine, Shelukindo aliiunga mkono Nec kwamba, kuna haja ya wabunge kudhibitiwa kwa sababu wengine wamefikia hatua hata ya kuwakejeli viongozi wa serikali badala ya kutumia hoja katika kujenga hoja.


Uamuzi huo wa Nec umetolewa baada ya mkutano uliopita wa Bunge kuwa moto kutokana na wabunge wengi, hasa wa chama tawala kuikalia kooni serikali, na hasa Baraza la Mawaziri wakilituhumu kwa kubariki mikataba ya ufisadi na kuweka kipaumbele kwenye miradi inayohusu maeneo yao.


Naye Dk Mahanga alielezea kufurahishwa uamuzi wa Nec wa kuzuia "wasema ovyo" katika vita dhidi ya ufisadi, akisema busara zake zilishaona hilo, anaripoti Leon Bahati.


Mahanga alijikuta kwenye kiti moto baada ya kuingilia mjadala wa hali ya CCM kwenye uchaguzi ujao, ambao ulianzishwa na makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Malecela ambaye alisema tuhuma za ufisadi dhidi ya wanachama wa chama hicho utawaweka pabaya baadhi ya wabunge kwenye uchaguzi wa mwaka 2010.


Mahanga, bila ya kuwataja waliomuunga mkono Malecela, alisema wale wanaotoa tuhuma za ufisadi bila ya kuwataja majina watuhumiwa, au kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria au kuwashtaki ndani ya chama, wanafanya kazi ya upinzani ya kuichafua CCM na hivyo akawashauri wajitoe kwenye chama hicho tawala.


Jana Dk Mahanga, ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, alisema suala hilo lilikuwa linamkera na kwamba uamuzi wa Nec wa kudhibiti wanaopinga ufisadi hadharani, ikiwa ni pamoja na kwenye vikao vya Bunge, umeunga mkono yale aliyoyaeleza.


Dk Mahanga alizungumza hayo kwenye mahojiano na gazeti hili jana, alisema kauli yake haikuwa ni utabiri bali ni busara ambazo mtu yeyote makini angeweza kuzitoa baada ya kutafakari mwenendo wa chama pamoja na vita dhidi ya ufisadi.


"Mtu yeyote ambaye anatafakari kwa makini jinsi hali ilivyokuwa, atakuwa na jibu kuwa suala la kuropoka ropoka tu na kutuhumiana kwa ufisadi, siyo njia sahihi na kamwe hakusaidii chama bali kukiharibu," alisema Dk Mahanga.


Njia sahihi, alisema, ni malalamiko kushughulikiwa kulingana na taratibu za chama na siyo kuyasema majukwaani ili kuufurahisha umma.


Baadhi ya wabunge ambao pia walizungumza na gazeti hili na kuomba majina yao yasitajwe gazetini kwa vile wao si wasemaji, walipinga vikali tamko la Nec.


Walisema suala la ufisadi siyo la kuficha na mbunge yeyote ana haki ya kufanya hivyo kwa maslahi ya wananchi.


Walisema suala la kufichaficha mambo na kuoneana huruma litaendelea kulea ufisadi na kwamba, atakayeumia ni mwananchi hasa wa kipato cha chini.


"Hivi mbona hatuwaonei huruma Watanzania hawa wanaovuja jasho kwa kodi, halafu lijitu, tena lenye uwezo wa kifedha linachukua mali zao na kujilimbikizia! Sisi viongozi ni lazima tufike mahali tuwaonee huruma walalahoi hawa," alisema mmoja wa wabunge hao.


Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa hata Spika Samuel Sitta ambaye alikuwa kwenye wakati mgumu wakati wajumbe wapatao 22, walipopendekeza atimuliwe kwenye chama, bado ana msimamo wa kuendeleza vita ya ufisadi.


Wakizungumza na gazeti hili jana, watu waliokaribu na Sitta walisema mbunge huyo wa Urambo Mashariki hawezi kudhibitiwa kwa kauli hiyo ya Nec, hasa ikizingatiwa analiongoza bunge kulingana na kanuni na taratibu ambazo zipo kwa mujibu wa katiba ya nchi.


"Mbunge hawezi kusimama kutoa hoja yenye maslahi kwa wananchi, halafu spika amuambie :"kaa chini!"


Alisema kitendo hicho kitakuwa ni udikteta na kuonya kuwa wabunge wana kanuni ambazo wanaweza kuzitumia, ili kumdhibiti spika.


"Kama kuna watu serikalini au wabunge wanaofurahia msimamo huo wa Nec, wajue wanajidanganya kwa sababu hauna nguvu yoyote ya kudhibiti uhuru wa bunge," alisema.


"Bunge lina nguvu ya kujadili mambo ambayo si spika wala Nec wanaoweza kuizuia."


Kuhusu tamko lililotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati kwamba "Bunge limeanza kuwa kama mchezo wa kikundi cha televisheni cha vichekesho kinachojulikana kama The Comedy, wabunge hao walisema kwamba hiyo ni dharau inayoonyesha kejeli, dhihaka na fedheha kubwa kwa bunge mbele ya wananchi.


"Kama suala ni uhuru ambao umefanya wabunge kuvuka mipaka na kila mmoja kuamua kufanya lolote bungeni, basi Nec isingesema na kuacha tu hewani. Ingeorodhesha kanuni zilizovunjwa na wananchi wakaelewa," alisema mmojawao.


Akitangaza maamuzi ya Nec, Chiligati alisema: "Bunge limeanza kuwa kama mchezo wa (kikundi cha televisheni cha vichekesho) The Comedy.


"Yaani kila mtu anafanya mambo yake mwenyewe, hali ambayo inaweza kusababisha watu kurushiana hata viatu ndani ya ukumbi wa bunge. Sasa hali hii maana yake nini?


"Kwa hiyo tumesema inatosha, hapo tulipofikia tusiendelee mbele. Wanaoropoka hovyo ni walevi na tumeona kuna kundi dogo ambalo limejiona kama ni wateule wa kuzungumzia sakata hilo (la ufisadi) bila ya kujua wabunge wote wana haki ya kuzungumzia suala hilo, lakini kwa utaratibu tena kwa kupitia katika vikao vya kamati za wabunge."

No comments:

Post a Comment